Ghana: Mfano wa kuigwa barani Afrika
Ghana ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizojaaliwa kugundua mafuta katika miaka ya hivi karibuni. Na tokea mwaka wa 2010 Ghana imekuwa inayauza mafuta hayo nje. Jee mafuta hayo yataleta neema kwa nchi hiyo ?
Jee vipi Ghana itaeweza kuepuka kinachoitwa laana ya raslimali ya mafuta ambayo nchi hiyo ilianza kuyauza nje tokea mwaka wa 2010? Jee viongozi wa nchi hiyo, kama wa nchi nyingine zenye mafuta nao pia watakengeushwa na lukuki za fedha zinazoingia bila ya daftari.? Na jee vipi matawi yote ya jamii,majimbo na kwa hivyo wananchi wote wataweza kunufaika na utajiri huo mpya?
Kwa Benjamin Boakye jibu la maswali hayo yote ni wazi! Mtaalamu huyo wa maswala ya uchumi amesema Ghana lazima izifuate sheria zake.Pana sababu kwa nini Ghana inahesabika kuwa nchi imara, na ya mfano wa demokrasia, katika eneo la magharibi mwa Afrika- sehemu isiyokuwa na utulivu.
Mtaalamu huyo wa masuala ya uchumi Boakye kutoka kituo cha sera za nishati cha mjini Accra,amesema sheria mpya za sekta ya mafuta nchini Ghana zinajumlisha taratibu zote za lazima zinazoweza kuchangia katika kuleta maendeleo yanayotarajiwa. Hata hivyo mtaalamu huyo ameleeza kuwa mafanikio yatatokana na utekelezaji wa taratibu hizo.
Dhamira ya Ghana
Mara baada ya Ghana kuyagundua mafuta kwenye pwani yake mnamo mwaka wa 2007,nchi hiyo ilidhamiria kufanya kila kitu kwa usahihi. Baada ya mashauriano ya kina na wataalamu wa ndani na wa kutoka duniani kote,Ghana iliupitisha mwongozo kamambe wa taratibu, kwa ajili ya sekta yake hiyo mpya ya uchumi. Sheria mpya juu ya ugawaji wa mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta, inaeleza wazi kabisa ,ni kiasi gani cha mapato hayo, serikali inaweza kutumia na kwa ajili gani.
Sera ya fedha za mafuta katika bajeti ya Rais Pamoja na mengine yote,inahakikisha kwamba mapato yanayotokana na mafuta yanaekezwa katika sekta za uchumi na katika majimbo yaliyomo katika orodha ya mambo ya kipaumbele. Sababu ya kufanya hivyo ni kuuepusha uchumi wa Ghana kunasa katika mtego wa kuitegemea sana sekta ya mafuta na kuzipuuza sekta nyingine za uchumi.
Awali ya yote ,sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa zaidi ya nusu ya watu wa Ghana lazima iendelezwe. Lakini mtaalamu wa masuala ya uchumi Benjamin Boakye amelalamika kwamba ukweli ni mwingine. Boakye aliyapiga darubini matumizi ya serikali ya miaka iliyopita. Ameweza kuziona fedha za mafuta ziliekezwa katika shughuli kadhaa za ujenzi wa barabara lakini ni katika majimbo ambayo tayari yana miundombinu bora,na siyo katika sehemu zilizokusudiwa, ambazo hasa zinavihitaji vitega uchumi. Boakye amesema,mbali na hayo,mapato yanayotokana na mafuta yameingia moja kwa moja katika bajeti ya Rais, aghalabu zaidi kuliko sekta muhimu kama vile ya kilimo.
Mwandishi wa kampuni ya Ujerumani ya kuhimiza biashara ya nje "Germany Trade and Invest" Carsten Ehlers anahofia kwamba kasoro hizo zinaweza kuwa mwanzo wa ufisadi wa kiwango kikubwa katika sekta ya mafuta nchini Ghana.Amesema kiwango kikubwa cha fedha za mafuta kitakuja kutokana na utaratibu wa kuyazingatia mahitaji ya kila sehemu husika.

Magari ya kusafirisha mafuta.
Mwanya wa rushwa
Kwa sasa Bunge la Ghana linaijadili sheria ya kuhimiza manufaa kwa wazalendo.Sheria hiyo itapasa kuhakikisha kwamba makampuni ya wazalendo yanashiriki katika sekta ya mafuta,kwanza kwa asilimia tano, na baada ya hapo kwa asilimia isiyopungua 60 hadi 90 ya sehemu ya mapato ya makampuni yote yanayozalisha mafuta nchini Ghana na yale yanayohusika na ugavi wa mafuta.
Mwandishi Ehlers anao wasi wasi hasa kwa kuwa,kwa mujibu wa mswada wa sheria husika,Waziri wa mafuta ataweza kuwachagua wajasiramali wa Ghana jinsi apendavyo .Utaratibu wa kuhimiza ushiriki wa wazalendo,aghalabu umesababisha kuongezeka kwa ufisadi na upendeleo katika nchi nyingine.
Lakini licha ya matatizo yote,mwandishi huyo Ehlers haamini iwapo Ghana itakumbwa na pepo mbaya wa mafuta ,kama inavyotokea katika nchi jirani ya Nigeria.Kwa mujibu wa makisio,kila mwaka dola hadi Bilioni sita zinaibwa kutoka kwenye mapato ya mafuta nchini Nigeria.Ghana bado ni ndogo mno kuweza kukifikia kiwango hicho,amesema Ehlers.Kwa mujibu wa takwimu rasmi,mapato ya Ghana yaliyotokana na mafuta,yalifikia dola milioni mia tano mwaka jana.
Ghana inazalisha mapipa zaidi ya 110,000, lakini bado ni chini ya asilimia10 ya mapipa yanayozalishwa na Nigeria, mzalishaji mkuu wa mafuta barani Afrika.Kiwango cha uzalishaji wa mafuta nchini Ghana kinaondoa wasi wasi wa kile kinachoitwa maradhi ya Uholanzi, amesema Ehlers.

Jamii ya Ghana ni yenye matumaini makubwa kufuatia kugunduliwa kwa mafuta.
Mauzo ya maliasilia nchini Uholanzi yaliyosababisha kuongezeka kwa thamani ya sarafu yaliziathiri sekta nyingine za uchumi wa nchi. Mtaalamu wa masuala ya uchumi Benjamin Boakye amesema kwa sasa bado ni vigumu kujua ni kwa kiasi gani, mafuta yameleta manufaa au madhara kwa watu wa Ghana.
Hata hivyo ametilia maanani kwamba angalau nchini Ghana upo mwongozo wa kuonyesha kimsingi, jinsi mapato yanayotokana ya mauzo ya mafuta yanavyoweza kuwanufaisha wote. Lakini Boakye amesema wajibu wa kuhakikisha kwamba mwongozo huo unatekelezwa, haumo katika mikono ya serikali tu. Ameeleza kuwa wanajamii wote wa Ghana wanapaswa kuhakikisha kwamba wanasiasa wanazifuata sheria.
Mafuta bado kuinufaisha Chad
Wakosoaji wanamueleza rais Idriss Deby wa Chad kwa maneno machache. Wapinzani wasiotakiwa nchini humo hunyamazishwa ama kununuliwa, na anafanya hivyo kwa kutumia mapato yatokanayo na mafuta.
Rais Idriss Deby wa Chad akishikana mikono na majenerali wa Chad katika jeshi la nchi hiyo lililoko Mali.
Kwa nje lakini rais Deby anajionesha kuwa ni mtu safi kabisa. Jeshi kama sehemu ya msaada katika masuala ya dharura , linatatua mizozo pamoja na wanamgambo katika maeneo ya magharibi na kati katika bara la Afrika. Hali inakuwaje katika ukandamizaji wa Deby ndani ya nchi hiyo na nguvu za kijeshi vikiunganishwa?
Katika orodha ya mataifa duniani Tchad licha ya kupata mapato makubwa kutokana na mafuta iko katika nafasi dhaifu sana. Katika kielelezo cha Umoja wa Mataifa kuhusu nchi zinazoendelea Chad iko katika nafasi ya 184 kutoka mataifa 187, ambapo nchi ambazo bado hazijapiga hatua kubwa katika maendeleo ni Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Niger.
Ukandamizaji wa haki za binaadamu
Matarajio ya watu kuishi nchini Chad ni karibu miaka 50, ambapo kila mtu mzima wa tatu anaweza kusoma na kuandika na asilimia 62 ya watu milioni 11 nchini Chad wanaishi kwa kutumia chini ya euro moja kwa siku. Haki za binadamu hukandamizwa, wapinzani hunyamazishwa, anasema Martin Petry, mshauri wa maendeleo wa kujitegemea na anaeifahamu Chad tangu miaka kadha iliyopita.
"Nchini Chad kama ilivyokuwa hapo kabla wapinzani wanakamatwa na kufanyiwa vitendo vya kikatili. Kumekuwa na matukio kadha ya kukamatwa , rushwa ndogo ndogo ni nyingi , na pia matumizi mabaya ya madaraka ya polisi, na wanamgambo. Iwapo mtu nchini Chad atanyimwa kuhusu haki yake, ni vigumu kuidai na kuipata tena," anasema Petry.
Rais Idriss Deby ameitawala nchi hiyo tangu mwaka 1990 na yuko madarakani sasa kwa muda wa miaka 23. Katika muda huu wa kuwapo madarakani , amekuwa akitofautiana kidogo sana na viongozi wengine wa mataifa ya Afrika kama vile Teodoro Obiang Nguema wa Guinea ya Ikweta , Jose Eduardo dos Santos wa Angola ama Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Wafanyakazi wa Chad wakielekeza bomba la mafuta katika kisima cha Doba kusini mwa nchi hiyo.
Fedha za mafuta zaimarisha uwezo wa jeshi
Jeshi la Chad ndilo jeshi lililopata mafunzo mazuri zaidi na lenye vifaa vya kisasa kabisa katika bara la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara. Hii imetokana na mapato ya mafuta ambayo yameanza kupatikana miaka kumi iliyopita. Helga Dickow , mtaalamu wa Chad kutoka taasisi ya Arnold-Bergstraesser katika chuo kikuu cha Freiburg nchini Ujerumani anasema.
"Fedha za mafuta zimemsaidia kujenga nguvu za kijeshi nje ya nchi . Chad kwa sasa ina jeshi lenye vifaa vya kisasa kabisa kusini mwa jangwa la Sahara. Kwa siasa za ndani lakini fedha za mafuta zimemjengea Deby madaraka makubwa ya kisiasa. Utawala wake una udhibiti kamili wa fedha zote za mafuta na unaweza kutumia fedha hizo kwa ajili ya kampeni za uchaguzi. Upendeleo na kuwatuliza wapinzani wa kisiasa ni mbinu kuu kama ilivyokuwa zamani."
Deby huwatumia watu anaowapendelea kuwakandamiza baadhi ya watu wengine. Hawa wanajulikana kutokana na kushirikiana kwa karibu na utawala huo. Wapinzani wa kisiasa wanavutwa upande wake kwa kuwapa nyadhifa za heshima na kuweza kuwaingiza katika mfumo wake wa utawala. Fedha nyingi hutumiwa nchini Chad katika ujenzi wa madaraka yake, lakini ni fedha chache zinazokwenda katika kupambana na umasikini ama ujenzi wa miundo mbinu.
Jeshi ambalo limeimarishwa kutokana na fedha za mafuta analitumia Deby kupata nafasi ya kutambulika kimataifa. Januari mwaka huu (2013)kwa mfano wakati rais wa Ufaransa Francois Hollande alipopeleka vikosi vya jeshi nchini Mali yeye aliweka tayari wanajeshi karibu 2,400 kutoka Chad .
Sera ya mambo ya kigeni ni muhimu
Akipambana na waasi wa Kiislamu na makundi ya kigaidi Deby anajaribu kupata kutambulika katika medani ya kimataifa na amefanikiwa katika suala moja. Chad inapata ukosoaji mdogo kuhusiana na siasa zake za ndani kuhusiana na uendeaji kinyume haki za binadamu.
Ni kwa kiasi gani mkakati huu wa Deby unavyofanyakazi, unaonekana pia katika mtazamo wa bara la Afrika binafs , kwamba sera za mambo ya kigeni ni muhimu , kama inavyooneshwa katika makubaliano yaliyofikiwa na Umoja wa Afrika, kwamba wanataka kuiunga mkono Chad katika kuwania nafasi ya kuwa mwanachama ambae si wakudumu katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa katika mwaka 2014 / 15.





No comments:
Post a Comment